Zoezi la kuhesabu kura baada ya uchaguzi mkuu Nigeria linaendelea huku matokeo ya awali yakianza kuripotiwa baada ya kufanyika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Rais aliye madarakani Muhammadu Buhari hakugombea baada ya kutumikia mihula miwili inayotakiwa. Mgombea wa chama cha All Progressives Congress cha Buhari ni Bola Tinubu mwenye umri wa miaka 70 huku Atiku Abubakar, 76, akiwa mgomea wa chama kingine cha jadi cha Nigeria cha People’s Democratic Party.
Tinubu ni gavana wa zamani wa Lagos na Abubakar makamu wa rais wa zamani. Mgombea wa tatu aliyeshangaza wengi katika mbio ni Peter Obi, wa Chama cha Labour, ambaye ni mashuhuri hasa miongoni mwa vijana.
Zoezi la kupiga kura Jumamosi lilikumbwa na ucheleweshaji mkubwa na mashambulizi katika baadhi ya vituo vya kupigia kura na hivi upigaji kura uliahirishwa hadi Jumapili katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kubwa ya Afrika Magharibi.
Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura imetabiriwa kuwa juu, hasa miongoni mwa vijana ambao ni karibu theluthi moja ya wapiga kura milioni 87 walio na sifa za kupiga kura. Uchaguzi wa Nigeria ni zoezi kubwa zaidi la upigaji kura barani Afrika na hivyo changamoto zilizoibuka zilitarajiwa.
Atiku Abubakar ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria, INEC, kutangaza matokeo haraka mara baada ya kusema baadhi ya magavana wa majimbo watajaribu kubadilisha matokeo hayo.
Mgombea wa urais anahitaji kuwa na ushindi wa asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika thuluthi mbili ya majimbo 36 ya Nigeria ili kutangazwa mshindi.
Kama kigezo hicho hakitatimizwa, kutakuwa na duru ya pili ndani ya siku 21 na iwapo hilo litajiri mwaka huu itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Nigeria.
Mbali na uchaguzi wa rais, Wanigeria pia wamepiga kura kuwachagua magavana, wabunge, maseneta na wajumbe wa mabaraza ya miji.